Matthew 19

1Ilitokea wakati Yesu alipomaliza maneno hayo, akaondoka Galilaya, na akaenda mpakani mwa Yudea mbele ya mto Jordani. 2Umati mkubwa ukamfuata, na akawaponya huko.

3Mafarisayo wakamjia, wakamjaribu, wakamwambia, “Je ni halali kwa mtu kumwacha mke wake kwa sababu yoyote?” 4Yesu akajibu na kusema, “Hamkusoma, kwamba yeye aliyewaumba mwanzo aliwaumba mume na mke?

5Na tena akasema, ‘Kwa sababu hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuungana na mke wake, nao wawili watakuwa mwili mmoja?’ 6Hivyo siyo wawili tena, bali mwili mmoja. Basi, kile alichokiunganisha Mungu, mtu yeyote asikitenganishe.”

7Wakamwambia, “Sasa kwa nini Musa alituamuru kutoa hati ya talaka na kumwacha?” 8Akawaambia, “Kwa ugumu wenu wa mioyo Musa aliwaruhusu kuwaacha wake zenu, lakini tangu mwanzo haikuwa hivyo. 9Nawaambieni, kwamba yeyote atayemwacha mke wake, isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, na akamwoa mwingine, amezini. Na mwanaume atakayemwoa mke aliyeachwa amezini.”

10Wanafunzi wakamwambia Yesu, “Kama ndivyo ilivyo kwa mume na mkewe, siyo vizuri kuoa.” 11Lakini Yesu akawaambia, “Si kila mtu anaweza kupokea mafundisho haya, bali ni kwa wale tu walioruhusiwa kupokea. 12Kwa vile wapo matowashi waliozaliwa tokea tumboni mwa mama zao. Na vilevile kuna matowashi waliofanywa na watu. Na kuna matowashi waliojifanya matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kupokea mafundisho haya na ayapokee.”

13Kisha akaletewa baadhi ya watoto wadogo ili awawekee mikono juu yao na kuomba, lakini wanafunzi wake wakawakemea. 14Bali Yesu akasema, “Waruhusuni watoto wadogo, wala msiwakataze kuja kwangu, kwa maana ufalme wa mbinguni ni wa watu kama wao. 15Naye akaweka mikono yake juu yao, na kisha akaondoka pale.

16Tazama mtu mmoja akaja kwa Yesu na kusema, “Mwalimu, ni kitu gani kizuri ninachotakiwa kufanya ili nipate kuwa na uzima wa milele?” 17Yesu akamwambia, “Kwa nini unaniuliza ni kitu gani kizuri? Kuna mmoja tu aliye mwema, lakini kama ukitaka kupata uzima, shika sheria za Mungu.”

18Yule mtu akamwuliza, “Ni sheria zipi?” Yesu akasema, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, 19waheshimu baba yako na mama yako, na mpende jirani yako kama nafsi yako.”

20Mtu yule akamwambia, “Mambo yote hayo nimeyatii. Bado ninahitaji nini? 21“Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze ulivyo navyo, na uwape maskini, na utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo unifuate.” 22Lakini kijana yule aliposikia yale Yesu aliyomwambia, akaondoka kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na amemiliki mali nyingi.

23Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kweli nawaambieni, ni vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni. 24Tena nawaambieni, ni rahisi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko kwa mtu tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”

25Wanafunzi waliposikia hivyo, wakashangaa sana na kusema, “Ni yupi basi atakayeokoka?” 26Yesu akawatazama na kusema, “Kwa wanadamu hilo haliwezekani, lakini kwa Mungu yote yanawezekana.” 27Kisha Petro akamjibu na kumwambia, “Tazama, tumeacha vyote na kukufuata wewe. Ni kitu gani tutakachopata?”

28Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, yeye aliyenifuata mimi, katika uzao mpya wakati Mwana wa Adam atakapoketi katika kiti cha enzi cha utukufu wake, ninyi pia mtaketi juu ya viti kumi na viwili vya enzi, kuwahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.

29Kila mmoja wenu aliyeacha nyumba, kaka, dada, baba, mama, watoto, au shamba kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia na kuurithi uzima wa milele. Lakini wengi walio wa kwanza sasa, watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.

30

Copyright information for SwaULB